Hello..!

Hii blog imeandaliwa kwa ajiri ya kuandika Hadithi (story) mbalimbali ambazo zitakua zinakufanya ufikiri na kuenjoy maisha... zitakufundisha, na kukupeleka mbaaali sana kifikra na kiupeo. Hadithi hizi nitakua ninazipost kila wiki mara moja, na kama kuna hadithi mtu utaipenda utawasiliana na mimi katika email yangu. (alpha2aaa@gmail.com )

Thursday, July 5, 2012

“I killed my best friend to complete Standard Seven, 1997” (Nilimuua rafiki yangu ili nimalize Darasa la Saba, 1997)

Dawa ya duku duku ni kulitoa lile lilioko moyoni, tena hasa hasa kama lile linalokusumbua ni la ukweli kabisa.  Ninachotaka kukisema hapa ni siri, siri ambayo imeutesa moyo wangu kwa zaidi ya miaka kumi na tano na sasa naona umefika muda wa kuutoa na kuutapika huu mrundikano wa uchafu moyoni mwangu.



Mwaka 1990 nilianza elimu yangu ya Msingi katika shule ya msingi Kichangani iliyoko Iringa mjini, na kama sio ajari mbaya ya gari ambayo niliipata mwaka huo huo 1990 basi ningemaliza elimu yangu ya msingi (darasa la saba) mwaka 1996 na rafiki yangu wa karibu sana “Charles Teonas Msimbwa” ambaye nilipoanza tu shule alitokea kuwa rafiki yangu wa karibu sana ambaya hadi tabia zetu zilianza kuendana. Urafiki wetu unadumu mpaka leo ingawa harakati za maisha zimefanya kila mtu apande boti yake na hivyo kuelekea uelekeo tofauti. Baada ya ajari hiyo mbaya nililazimika kuacha shule na kuendelea na matibabu yaliyochukua takribani mwaka mzima.



Mwaka 1991 nilianza tena elimu ya msingi, hapo ndipo nikakutana na marafiki wapya kama vile Ezekiel Chongola, Lusjoy Mgimba, Bernivenuth Joseph, Amos Malipula, Rogers Lobert, Ahmed Kalenga, Moses Chengula, King Nindie, Moses Mkanumkole na wengine wengi sana ambao kama nitaamua kuwataja wote, basi utaacha kusoma hii story kwani nitaishia kukuboa tu. Wakati huo Charles alikuwa darasa la pili na hivyo akawa kama kaka angu wa shule na pia rafiki yangu mshauri, tena mshauri wa karibu aliyekuwa akinishauri kila janbo zuri na baya.



Nilianza shule nikiwa mwema sana (mtoto mzuri), lakini kadili miaka ilivyosogea nilianza kuwa mtukutu sana, hii ilitokana na kupona kabisa majeraha na kusahau baadhi ya makovu ambayo nilisababishiwa na ile ajari mbaya ya mwaka 1990, sio kwamba zamani kabla ya hapo sikuwa mkorofi, laa... hata hiyo ajari ya kugongwa na gari ilitokana na utundu uliokithili ambao kwa namna moja ama nyingine naweza kusema ulinicost sana, ila baada ya kupona nahisi nilisahau maumivu na kuwa mtundu zaidi kiasi cha kuanza kuwa kero kwa baadhi ya watu. Nilikuwa napenda sana kupigana hasa kwa kutumia siraha kali, kuruka sarakasi za hatari, kuogelea kwenye kina kirefu, kudandia magari, michezo ya kivita, gholofa la shule ya msingi la kichangani nilikuwa naliona fupi tu, halikunitisha sana na kila siku nilikuwa natamani kujaribu kuruka kutoka juu ili nijipime uwezo.



Nilipofika darasa la tatu (1993) ndipo nikaanza utolo, nilianza kutoroka shule na kuingia chaka ama pori. Kawaida tulipenda sana kwenda kujificha juu kabisa, juu ya jiwe kubwa karibu kuliko mawe yote mkoani Iringa (Jiwe Gangi) jiwe hili lipo Gangilonga. Huko tulikuwa tunakutana na watoro wenzetu wooote wanaosoma shule zinazoizunguka Iringa mjini, huko tulipenda sana kucheza kamali, kupigana, kuvuta bangi na mambo mengine mengine ya kihuni ambayo mengineyo yalikuwa yametuzidi hata umri wetu. Huko kwetu kulikuwa ni mahali salama kwani hakuna mtu ambaye aliwahi kuthubutu kuja kutufuata, iwe ni mzazi, mwalimu, kilanja ama police wote walikuwa waoga kupanda jiwe hilo ambalo licha ya kutisha na ugumu wake wa kupanda jiwe hilo pia tulikuwa na tabia ya kuwapopoa na manati ama kuwarushia mawe na kuwafanya waone si mahali salama kuja. Wakati mwingine tulikuwa tunaenda kuogelea katika mto ruaha ambako pia matendo yetu yalikuwa yale yale tuliyoweza kuyafanya juu ya Jiwe Gangi. Huku pia tulikutana na vibaka wa mjini na wanafunzi wenzetu kabao ambao woote pia wametoroka mashuleni kwao. Ilikuwa kama chuo kingne ambacho kilikuwa kinanifundhisha mambo mengi sana tena kwa vitendo. Huku nilikuwa najifunza haraka kuliko hata shule ambao nilikuwa naona kama vile nadanganywa tu, kuambiwa mambo ya pai, vipeuo vya pili, asidi, litimasi ya bluu na nyekundu na vitu vingine vingine ambavyo hata nikimuuliza mwalimu swali vingine alishindwa kunipa majibu fasaha.



Mama yangu ambaye alishaanza kugundua mmomonyoko wa maadili yangu na maendeleo yangu mabovu shuleni, alianza kunifuatilia bila kupata majibu, kwani nyumbani nilikuwa naondoka kila siku kwenda shuleni, na kila siku shuleni nilikuwa nafika, ten nilikuwa napiga sana ngoma katika gwalide la shule baada ya kuimbisha sana nyimbo katika mchaka mchaka ambao tulikuwa tunakimbia kutoka Kichangani mpaka Gangilonga, mara nyingi katika mchaka mchaka huu ndipo tulipokuwa tunapata upenyo wa kutoroka na kuingia porini. Lakini mimi mara nyingi nilikuwa narudi hadi mistarini (Assemble) ambako nilikuwa nahudhuria hadi kipindi cha ukaguzi wa usafi ma mambo mengine mengine halafu tunapoingia darasani hapo ndio na mimi nachomoka na kwenda kwenye darasa langu. Huu ushauri wote pia nilikuwa naupata kutoka kwa Charles ambaye kipindi hicho yeye alikuwa darasa la nne. Kwa hiyo mama yangu alibakia tu kuilaumu shule kuwa huenda wakawa hawafundishi vizuri kwani alikuwa anaamini kuwa mimi nina akli sana, aliamini kuwa mimi niana uwezo mkubwa sana wa kuelewa kwa hiyo kupungua kwa maendeleo yangu shuleni aliamini kuwa ni tatizo la waalimu na sio mimi, masikini mama yngu… hakujua, hakujua kuwa akili yangu niliihamisha na kujifunza skills nyingine kabisa katika maisha, hakujua.



Marafiki zangu wa kijiwe walitokea kunipenda sana, ikawa endapo sijatoroka shule walikuwa wanakosa raha kwa kunikumbuka, wengine walikuwa wanadiliki kurudi hadi shuleni na kunishawishi nitoroke ili kijiwe kiendelee kuwa imala siku zote… nilikuwa na kipaji cha kupasha stori kilinge kizima nao wakawa wanafurahia sana. Wakati mwingine nilikua naanza kusimulia hadithi ambayo hata mimi mwenyewe sijui inatoka wapi na sijui itaishaje… kwa hiyo hata mimi pia nilikuwa najifunza kutoka kwenye strori zangu mwenyewe na pia kuzifurahia. Hiki ndicho kitu pekee kilichofanya hawa watu wanikumbuke sana kipindi ambacho nidhmu ya shule ikipanda na kuongezea mahudhurio, wakawa wanakosa utamu, vicheko na kupoteza muda vizuri.

Pia nilikuwa mtaaramu sana wa kutengeneza kijiti (ku roll bangi), kuviringisha bangi kwenye lizla. Kila nilipo roll mimi wavutaji wengi waliifurahia sana hiyo bangi kwamba ina mzuka sana, ingawa kitu cha ajabu ni kwamba mimi mwenyewe sikuwahi kuvuta hiyo bangi wala sigara, nadhani hii ilitokana nah ii aleji ya moshi niliyokuwa nayo, ambayo nikisikia harufu hiyo huwa najisikia vibaya sana. Pia rafiki yangu Charles hakupenda kabisa mimi nivute bangi wala sigara, pia hakupenda kabisa ninywe pombe, hata yeye hakutumia kabisa hivi vitu. Niliweza pia kujizuia kuto tumia vitu hivi ingawa kwenye pombe hapo nilishidwa kabisa hivyo nikawa naipiga, tena ki sawa sawa.





Kipindi hiki chote nilikuwa naitwa Alpha Said, na hili nio jina ambalo watu wengi niliosoma nao walilifahamu sana, darasani na vyeti vyangu vilitambulika hivyo, leo hii jina hili halipo tena, naitwa Alpha Ambokile… kuna mambo mengi yamejificha nyuma ya mabadiliko ya jina hilo na historia yangu pia, kama nikitaka kuandika yote itabidi kiwe kitabu na itakuchukua muda mtrefu pia kunielewa. Hauwezi kunielewa mimi kwa siku moja tu, kwani unionavyo sasa ni matokeo ya mambo yaliyojijenga kwa zaidi ya miaka 25…! Kwa hiyo anayesimulia hii story sasa ni Alpha Ambokile na sio Apha Said tena kwa hiyo nawaomba jamani msije mwisho wa siku mkanihukumu mimi ‘Ambokile’ kwa makosa aliyoyafanya ‘Said’.

“Nipo Kaanani sasa, usinihukumu kwa mambo niliyoyafanya Misri”



Ingawa nje ya darasa wanafunzi wenzangu walikuwa wananiita “FUMO”. Hili jina nilipewa kutokana na umahiri wangu wa kusakata kambumbu, kipute ama soccer nilipokuwa uwanjani. Nilikuwa nakimbiaza sana winga zote mbili kulia na kushoto hivyo marafiki zangu wakaamua kuniita jina la Fumo kwani waliniringanisha na “Fumo Felistian” mcheazji aliyekuwa machachari sana ambaye aliichezea Pamba na Yanga kipindi hicho. Sijui kwa sasa mchezaji huyu mahili yuko wapi ila nilikuwa napenda sana kumwona katika maisha yangu.



Maajabu ya shule niliyokuwa nasoma nilianza kuyaona na kuyagundua nilipofika darasa la nne (1994) ambapo mwanafunzi mmoja wa darasa la saba alifariki dunia katika mazingira ya utata sana, shule ilipofungua tu mwezi wa kwanza mwanafunzi huyu mabaye sikuwa namfahamu kwa sura alikuja darasani kabisa, ilipofika mida ya saa nne na nusu, kipindi cha mapumziko jamaa alianguka darasani na kukata roho. Niliumia sana roho, wanafunzi wote wa Kichangani tuliguswa sana na msiba huo. Ndipo nilipoambiwa kuwa hilo ni suala la kawaida kutokea katika shule hiyo. Niliambiwa kuwa kila mwaka unapoanza ni lazima mwanafunzi mmoja wa kiume afe, tena ni lazima awe ni mwanafunzi wa darasa la saba.



Moyo wangu ulianza kuugua taratibu baada ya kuijua hiyo historia mbaya ya shule yetu nzuri, shule ambayo tulikuwa tunaamini ni shule nzuri kuliko shule zote za msingi za Serikali katika manispaa ya Iringa. Shule ya mazoezi ya kichangani, ambayo ilikuwa chini ya chuo cha ualimu cha Kreruu na kuifanya iwe na sifa tele. Waalimu walipokuwa wakifanya mazoezi ya vitendo basi walikuja kutufundhisha sisi. Wanafunzi walikuwa wanafaulu sana katika mitihani yao ya mwisho na kufanya waalimu wajisikie na kujivunia kufundhisha shule hiyo, wanafunzi pia tulijivunia sana kusoma hapo shuleni. Darasani tulikuwa hatufiki hata wanafunzi 80, na kulikuwa hakuna mikondo (Steems) kwa hiyo shule nzima tuliweza kufikia idadi isiyozidi hata wanafunzi 560 tu, kwa hiyo kwa mwalimu mwenye kumbukumbu nzuri kama Mwl. Mwalongo aliweza hata kutufahamu hadi kwa sura na majina wanafunzi wote ingawa sisi watoro watoro ndio tulikuwa tumamuumiza sana kichwa kwani aliishia kuyajua majina tu sura hakuwahi hata siku moja kuzijua. Hii ilitokana na tabia yetu ya kuchukuliana adhabu, yaani wakati mwingine kosa kafanya Ahmed Kalenga lakini akikamatwa anataja jina la Ezekiel Chongora, mwalimu akija darasani kumuita Ezekiel Chongora ili amchape ama kumpa adhabu basi anaenda mbele Alpha Said, anapewa adhabu, ama kuchapwa basi. Sisi wanafunzi (watoro) tunabaki na madeni yetu na tulikuwa tunajuana wenyewe. Siku nyingine mimi nikitakiwa kupewa adhabu basi mwenye deni langu anaenda kuchukua badala yangu na tulikuwa na system nzuri kwani hatukuwahi kudhulumiana katika hili.

Kwa hiyo historia hii chafu ilianza kunifanya nijutie kusoma kichangani.



Kulikuwa na uvumi kwamba, miaka ya 1980 kuna wanafunzi wakiume walitoroka na kwenda maeneo ya Makanyagio, maeneo ambayo katika historia ya Tanzania na Iringa yanamuhusisha sana Mtwa ama Mtemi Mkwawa wa Kalenga. Huko wanafunzi hao walivamia shamba la Mihogo na karanga, mali ya bibi kizee mmoja na kuanza kuiba. Walihalibu sana shamba la bibi huyo ambaye alikuwa akikaa peke yake baada ya kufiwa na wanawe na ndugu zake kumterekeza. Kibibi huyo alikuwa akijishughulisha na kazi zake za shamba wakati akisubiri siku yake ifike. Inasemekana kwamba bibi huyo alipogundua kuwa waliomuibia ni wanafunzi wa shule ya kichangani alijitahidi na kufika shuleni hapo ambapo alidai alipwe fidia ya uhalibifu wa mali yake uliofanywa na wanafunzi hao lakini mkuu wa shule aliyekuwepo kipindi hicho alimfukuza kwa dharau na kudai kuwa wanafunzi wa shule yake hawawezi kufanya ujinga kama huo… alimfukuza na kumwambia aende huku huko kwenye shule za kishenzi akatafute wezi wake na sio shule ya kichangani ambapo watoto wengi wanaosoma hapo wazazi wao walikuwa na uwezo mzuri sana kiuchumi. Inasemekana kwamba bibi huyo aliondoka kwenye viwanja hivyo vya shule huku akiwa na majonzi tele kwani alikuwa na uhakika na kile alichokuwa akidai.



Bibi huo mzee sana, aliamua kufanya kitu ambacho kingefanya wanafunzi hao wamkome bila kujari kwamba walihusika na wizi huo ama laa, bora tu wanasoma Kichangani… basi alienda akafanya “Tego” la kishirikina ambalo lilikuwa linamuua mwanafunzi mmoja wa kiume ambaye anakaribia kumaliza shule kila mwanzo wa mwaka, na aliamua kufanya hivyo mpaka kipindi ambapo mwalimu mkuu yule angegundua na kwenda kumuomba msamaha bibi kizee.

Kwa bahati mbaya bibi huyo alifariki dunia mwaka unaofuata kabla hata mwalimu mkuu hajagundua kuwa lile ni tatizo kubwa na kufanya kila mwaka unapoanza basi ni lazima mwanafunzi mmoja wa darasa la saba afe.



Mwalimu mkuu huyo pia aliahamishwa kutoka shule hiyo na kupelekwa Sumbawanga miaka hiyo hiyo ya 1980 bila kujua huku nyuma ameacha tatizo ambalo lilijawa na utata mkubwa sana.





Kitu kilichoendelea kunishangaza na kuniumiza zaidi moyo ni pale ilipofika dalasa la tano (1995) ambapo tena ilitokea mwanafunzi mwingine wa dalasa la saba wa mwaka huo alifariki dunia tukiwa uwanjani tunacheza mpira mara tu baada ya shule kufungua. Hapo ndipo nilipoona kuwa nimeanza kuwa mkubwa kwani nilianza kuhisi vizuri maumivu ambayo mwnadamu anayapata baada tu ya kufiwa na mtu wa karibu. Niliogopa sana na kuwa natetemeka kipindi chote cha msiba ambacho sisi wanafunzi wa kichangani tulikuwa mstari wa mbele sana katika kumzika rafiki yetu huyo mpendwa. Hapo ndipo nilipoanza kuamini ule uvumi wa bibi kizee na kunifanya niwe muoga zaidi.



Kwa wanafunzi suala la kifo kwa mwanafunzi mmoja wa kiume wa dalasa la saba lilianza kuwa suala lililozoeleka na kuliona ni kitu cha kawaida isipokuwa kwangu mimi… mimi bado niliona kwangu ni mtihani mzito ambao nilikuwa natamani sana kuuukimbia na kuuepuka kabisa. Kila nilipomuomba mama yangu anihamishe shule aliniona naongea upuuzi kwa kuwa yeye alidai haamini kabisa imani za kishirikina, pia alidai kuwa Kichangani ni shule bora zaidi ya zote ambazo mimi nilipendekeza… wanafunzi wengi sana walio amini uvumi ule kama mimi waliihama shule ile na kukimbilia mbali.



Kitendawili kilikuwa nani atakufa mwaka unaofuata… mwaka wa kina Charles kufa ama kumaliza shule ulikuwa unasogea kwa kasi sana huku kila mwanafunzi wa kiume akiwa amejawa na hofu ya kifo cha ajabu… sisi tulikiita “kwenda kwa bibi” kwa hiyo kitendawili kilikuwa ni nani ataenda kwa bibi mwaka huu… hicho ndio kilikuwa kitendawili cha miaka yote kila mnapokaribia kufika darasa la saba. Ilifikia hadi atua ya kuanza kupigiana Kura wenyewe kwe wenyewe na mwanafunzi mwenye kura nyingi mara nyingi ndio huyo huyo pia alikuwa anaenda kwa bibi (kufa) yani utadhani tego hilo lilikuwa linazipata kura hizi mbaya za wanafunzi.



Kwa hiyo tulikuwa tunapigia Kura dawati moja ambalo bibi atamchukua mtu mmoja kwakuwa tulikuwa na utaratibu wa kukaa wanafunzi watatu kila dawati na hawa watu watatu mtakaa hivyo hivyo mpaka mnamaliza shule, utaratibu huu uliwekwa na Mwl. Mpako mwalimu aliyekuwa fundi stadi wa kuchapa bakora za matakoni. Alipenda kufanya hivyo ili kutukamata watoro kwani akiingia tu darasani akiona dawati limekaliwa na mtu mmoja basi alikuwa anambana huyo mpaka ataje rafiki zake wawili waliko na hivyo akawa anatukamata kirahisi sana.

Kwa hiyo Kura zikishapigwa basi tulikuwa tunaamini katika dawati ambalo kura nyingi zimedondokea basi huenda bibi akapita hapo na kumchukua mtu wake, mara nyingi sana kura hizo zilifanya kazi kweli inagawa mara nyingine alitoka mtu tofauti.



Mwaka 1996, nilipokuwa naingia darasa la sita, tunapofungua shule hari ilibadilika kidogo. Hapa tukajua bibi ametusamehe na mkosi umekwisha, kwani mpaka wiki ya tatu inakatika hakufa mwanafunzi yeyote yule. Hata rafiki yangu Charles nikaona furaha yake ambayo ilikuwa imempotea kwa kipindi chote cha likizo ya mwezi wa 12 na krisimasi, wakati akisubiri kujua nani atakwenda kwa bibi ilianza kumrejea tena. Ingawa Charles hakupigiwa Kura yeye wala dawati lake lakini alikuwa muoga sana, alidhoofu sana mpaka mimi muoga mwenzake ndio nikawa mfariji wake katika kipindi hicho kigumu. Waalimu na wanafunzi wote tulishangaa kuona mwaka huu unaenda salama na kuanza kuendelea na michakato ya kielimu kama kawaida.



Wiki ya tatu ya mwezi wa kwanza ndipo ikaanza mitihani ya ‘ujirani mwema’ kwa kaka zetu wa darasa la saba (kina Charles), mitihani ambayo ilikuwa inaunganisha shule kadhaa kama vile Kichangani, Wilolesi, Kihesa, Gangilonga na nyinginezo za pale Iringa mjini. Basi tuakasahau majanga na kukaa katika mkao ama ‘pozi’ la kimitihani ambayo tulikuwa tunaiheshimu sana kwani ilikuwa ndio kipimo cha kwanza kwa dalasa la saba, mitihani hii ilipendwa kutokana na ushindani uliokuwepo baina ya shule hizi zilozopo Iringa mjini. Pia ilikuwa ndio mitihani pekee ya kwanza kujua madudu na mazuri ni yapi kwa kila darasa la saba.





Wakati mtihani unaendelea… katika chumba cha mtihani, mwanafunzi mmoja wa kiume (Leonard Mgeni) alianguka darasani na kufa hapo hapo. Huyu sasa alikuwa rafiki yangu zaidi kwani alikuwa karibu sana na Charles na mara moja moja tulikuwa tukitoroka wote. Hapo ndipo taswila ya bibi iliporudi na gumzo kuendelea kutawala akili za waalimu na wanafunzi, hasa hasa sisi tunaokuja nyuma kwani kwa darasa la saba wenyewe (Boys) hufurahia kupona kwenda kwa bibi, lakini pia husikitika sana kwani wamempoteza ndugu yao mpendwa.



Kama kawaida tulifanya mazishi na kuendelea kuumia miyo yetu kwa mwaka mzima. Mimi moyo wangu ulikuwa unaniuma zaidi kwani nilikuwa ninashikwa na hofu kubwa sana kuhusu nani atakayefuata…

Mwezi wa sita ndio mwezi ambao mara nyingi tulikuwa tunaazna kubashiri nani atafuata na kuanza kupiga hizo kura mbaya. Mimi katika dawati langu nilipenda sana kukaa na Ezekiel Chongora na Lusjoy Mgimba. Mimi nilikuwa napenda sana kukaa katikati ya hawa watu wawili kwani ilikuwa inaniongezea kijiamini (Confidance) sana nikiwa katikati kuliko nikiwa pembeni.. Kwenye yale masuala ya chabo na kuficha uchafu na kptula yangu ambayo mala nyingi ilikuwa inatatuka pembezoni mwa mapaja yangu kutokana na kutuka sarakasi na kupiga mashuti nikiwa kiwanjani nasakata kandanda. Wenzangu hawa wawili na mimi pia wote tulikuwa watoro sana na kufanya dawati letu kuwa maarufu sana kwani tukitoroka wote tunakusekana na kufanya dawati liwe tupu hivyo Mwl. Mpako alikuwa anagundua mapema sana kila anapoingia darasani. Pia tulikuwa tumekubuhu kwenye ule mtindo wa kugandisha fimbo, yani mwalimu akiwa anakuchapa hautikisiki mpaka anamaliza hata kama itapiga fimbo kumi.



Kura za kwa bibi zilidondokea kwenye dawati letu. Hapo ndipo nilipoanza kuuamini ule wasi wasi wangu uliokuwa unanishika kila mara kwamba huenda ukawa na sababu, nilibadilika ghafla na kuanza kuwa mwema sana, ghafla nikaacha utoro na kuwa na mahudhurio mazuri sana darasani. Nikaanza kufaulu vivuri sana darasani na kuwafanya wanafunzi wenzangu waanze kunishangaa…! Mwalimu Mwaikeja, aliyekuwa akifundisha hesabu alianza kunisifia sana darasani na kufanya watu wote wawe wananiangalia mimi, kila mtihani unapofanyika, yanapotoka majibu watu wanataka kujua Alpha Said kapata ngapi..!!? Hiki kitu kilikuwa kinawashangaza sana Lusjoy na Ezekiel ambao walikuwa wananiona mimi ni Geniusn sana, ingawa sikuwahi kumpita mtu kama Amos Malipula, King Nindie na Rogers Lobert Gregory ambao walikuwa moto wa kuotea mbali lakini na mimi nilikuwa natetemesha watu kutokana na mabadiliko na maendeleo yangu ya kasi ya ajabu. Wazazi nao wakaanza kujenga matumaini mapya juu yangu na kuanza kuahidi kuwa watajinyima vyovyote vile waezavyo na kuhakikisha kuwa watanisomesha kwa nguvu zao zote na kuhakikisha kuwa nitasoma mpaka namaliza Chuo Kikuu ingawa swala la kuhama shule kwao ilikuwa ni sawa na kuongea lugha ambayo haitambulikani duniani.



Mwezi wa kumi na moja ukafika, kina Charles wakamaliza shule na kuondoka, sisi pia tukafunga shule huku watu wote wakiwa wamebaki na hiki kitendawili, nani ataenda kwa bibi mwezi wa kwanza mwakani??



Siku ya kufunga shule kwa darasa la saba ilikuwa ni siku ya majonzi sana, mara zote tulikuwa tunaitana wanafunzi wote wa kiume na kupeana moya na nasaha za mwisho kwani wakati mwingine huo ndio ulikuwa unakuwa mwisho wa kuonana kwani wengine walikuwa wanahama shule ama laa tunapofungua tu shule basi mmoja kati yetu hufa. Tulikuwa tunakaa pamoja, tunaagana na kupeana moyo kwamba kifo ni kitu cha kawaida na kwamba mti yeyote kinaweza kikamkuta wakati wowote. Maneno ambayo kwangu mimi bado hayakunipa ,oyo hata kidogo, ila bado niliendelea kuamini kuwa hii sasa ni zamu yangu mimi… na nilikuwa naona kama hawa jamaa na marafiki zangu sasa ndio nawaona kwa mara ya mwisho, machozi yalikuwa yakinilenga lenga na kujihisi kama homa kali ikininyemelea. Nilijiona naweza hata kufa kabla ya shule kufungua.



Baada ya kuagana na wavulana wenzangu ndipo tukakutana na Ezekiel na Lusjoy, yaani sisi ambao kura ya ndio imedondokea kwenye dawati letu, sisi pia tulikuwa na kikao chetu ambacho pia tulikuwa tunapigiana kura kwamba nani afe kati yetu sisi watatu, no sio afe, aende kwa bibi… hilo ndio lilikuwa neon lahisi sana kutumia kwa kipindi hicho.



Tulipokaa wenyewe chemba, baada ya kupeana moyo tuliamua kupiga kura. Kila mmoja alitakiwa kumshika bega mwenzake ambaye yeye alihisi labda huyo hasa ndiye ambaye angeenda kwa bibi mwakani… kitendo hiki huwa kinafanywa mara moja tu, tena wazi wazi na hakirudiwi tena. Hapo ndipo mambo ya ajabu yalipoanza kunitokea mimi.



Mimi kwa haraka sana bila hata kujijua nikajikuta mkono wangu wa kulia umetua begani kwa Lusjoy Mgimba, na wale wenzangu wawili wote kwa pamoja wakanishika bega mimi. Kwa hesabu za kidemokrasia hii ilimaanisha kwamba Mimi ndio niliyepigiwa kura kwani Ezekiel hakupata kura yeyote (0), Lusjoy alipata kura moja (1) na mimi nikapata kura mbili (2) yaani za kwao zote na hapo mchezo ukaisha. Basi shule ikafunga na tukatawanyika.



Nilipokuwa njiani narudi home ndipo nikaanza kuuona uzuri wa dunia hii, uzuri wa maisha, magari, majumba, ndege, wanyama, mimea, upepo na kila kitu kilichoijaza dunia nilianza kukiona ni kizuri na kinapendeza sana… nilikuwa naongea peke yangu, najiuliza maswari na kijibu mwenywewe huku nikicheka kupiga makofi, kushangaa ama kulia. Watu wasioelewa chochote walikuwa wananiona kama uchizi ndio huoooo unaninyemelea. Nilikuwa kama mtu mwenye kisirni na hasira kali kwa kila ninayemuona mbele zangu.



Nilipofika home jioni, huku nikiwa mchovu sana nikajifungia chumbani kwangu na kuanza kuwaza kwa kina nini nifanye ili ikiwezekana kikombe hicho kiniepuke, nikajikuta ninamchukia sana bibi. “Why me Lord” hili ndio swali la kwanza kuanza kujiuliza kichwani mwangu tena kwa lugha ya kiingereza. Nimekukosea nini Mungu? Kwanini mimi? Kwa nini kura zinidondokee mimi? Katika wanafunzi wote 80… kwa nini Alpha Said?



Jioni ya siku hiyo sikuwa na hamu ya aina yeyote ya chakula lakini nilienda sebureni ili ku zuga watu wasijue chochote, lakini nilikua kama mtu ambaye ametoroka hospitalini huku akiwa na homa kali sana, mwili wangu wote ulikuwa unatetemaka kwa hofu huku jasho jembamba likiwa linanitoka…. Ile baridi ya Iringa inayosifika siku hiyo sikiiona kabisa lakini nilikuwa nahisi joo kali kuliko hata la Dar na wakati huo huo natetemeka sana. Mama Alpha (mama), aliponoiona tu aligundua tatizo lilolokua linanikabiri. Nikagusa gusa vyakula vyao pale mezani na kuamua kudanganya kwamba nimekula muda si mrefu hivyo siwezi kula tena, huku nikiwa naimani kuwa hakuna anayeelewa badiliko lolote kwangu (Niko normal). Mama akaniambia usiende kulala nataka kuongea na wewe subiri nimalize kula.

Nikakaa kando kidogo huku nikimuangalia mama kwa huruma,

“Masikini mama yangu, namuacha peke yake na watoto wake wa kike, atalia vipi siku ya mziba huyu mwanamke…!? (Nilijiuliza kichwani) tena ukizingatia mimi ni motto wake wa kwanza, tena wa kiume pekee na mume wake aliisha kufa na kumuacha mjane… ni vipi ataupokea huu msiba ambao kwake utekuwa ni msiba mzito ambao utamtesa kwa kipindi chote cha maisha yake yaliyobaki. Nilikuwa najua wazi ni jinsi gain mama yangu ananipenda sana, tena kuliko hata watoto wake wote watano. ‘Kweli vipendwavyo huondoka mapema’ niliendelea kufanya mjadala mimi na moyo wangu mwenyewe.” Kabla sijasikia huyu mama anataka kuniambia nini…



Alipomaliza kula akaja na kunishika begani, “nakupenda sana mwanangu, nenda kalale baba yangu… kama kuna mtu kakuudhi msamehe”. Kumbuka kusali kabla hujalala. Hicho ndicho kitu ambacho mama yangu alisema baada ya kumsubiri kwa takribani nusu saa. Bado nilimuona mama huyu kapungukiwa uono, nilimuona bado haelewi kitu chochote katika hii dunia ambayo mapana yake hayana mwisho…! Sikuona nilichokipata katika kauli yake, nikamuaga nakuingia kwangu chumbani.



Sikuwa na jinsi, niliamini tu kwamba ni lazima nife, nilikumbuka jinsi rafiki yangu Charles alivyorejewa na ruraha mara tu baada ya rafiki yake kufa pindi walipoingia darasa la saba na kukumbuka kuwa “inabidi mmoja afe ili wanaobaki waishi kwa amani” hili kwangu kwa sasa lilikuwa ni suala amboalo hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kulipinga…. Katika kila kiwango (level) ya maisha nilianza kuona hili suala lipo, lazima mtu mmoja ateseke, aumie au afe ili wanaobaki waishi kwa amani, ila tatizo sasa sisi wanadamu ndio hatuko tayari kufa ili kuponya wengine watakao baki.



Siku za rikizo zilipokuwa zinakaribia kuisha ndipo nikaona muda wangu wa kufa unakaribia. “Muda wa kufa unapokaribia ndipo uzuri wa dunia hii unapoanza kuonekana dhahiri” nilitamani sana siku zigande, ama zirudi nyuma kabisa. Likizo ya mwezi wa kumi na mbili ni likizo ambayo wanafunzi wote wa Tanzania huifurahia sana, kwani ni likizo ambayo licha ya kuwa na sikukuu nzuri katikati yake ila inapoisha wanafunzi hupanda vidato. Kwangu mimi ilikuwa ni likizo ya majonzi na majuto.



“Aliwazalo mjinga ndilo litakalo mtokea” hii kauli ilinifanya nijaribu kujisahaulisha kwamba mimi sio chaguo la bibi la mwaka ujao, niliamini kabisa kama nitaendelea kuwaza na kuamini juu ya hili suala nitakufa kweli. Lakini kila nilipokumbuka zile kura…. Daaaah….! Niliendelea kujua ni mimi tu…. Ni mimi ndiye niliyehukumiwa,  “nilihukumiwa hukumu ya kifo kwa kosa mabalo katu sikuwahi kulifanya” nilihisi kuanza kuwachukia marafiki zangu. Kweli usiku huo nilisali kabla ya kulala huku nikiwa na hofu kubwa isiyopimika “Asiye amini uchawi, ushirikina na kazi nyingine zote za Shetani sidhani kama atamwamini Mungu vema” nilazima uamini, lazima ujue hivi vitu kweli vipo ndipo utakapo ona haja ya kujiweka karibu na Mungu.



Zilibaki wiki mbili ili shule ifungue, nilikonda sana, nilidhohofu mwili na kuonesha kila dalili ya kukata tama… “Kama imani yako yaweza kukuponya basi yaweza kukuua pia” inategemea na jinsi mtu unavyoamini pia ni nini unachoamini… hii ilidhihilika kwangu ambaye niliamini lazima nife. Nilijiuliza maswali mengi sana… Sasa kama nikifa nitaenda wapi…!? Kwa bibi kweli…!? Ama…!! Hapo ndipo nikaamini kuwa wanadamu hatuogopi kifo kwa kuwa tukienda haturudi, ila tunaogopa kwa kuwa hatujui tukifa ni wapi tunakwenda. Lakini pia nilijiuliza… Mungu analichukuliaje hili suala la mtu kufa kila mwaka? Kwa nini anaruhusu ili suala litokee…!!!? Je haelewi tabu kama hii ambayo mimi ninaipata…!!!? Kama nikifa….!!!! Huo ndio ulikua mwanzo wa kila aina ya swali ambalo nilikuwa najiuliza kwa kipindi hiki.



Kufikilia kifo kila mara kulinikengeusha moyo wangu, ukafika wakati nikaingiwa na roho ya kinyama, hapo ndipo uwanadamu uliponitoka na kuvaa roho ya kikatili, sikuogopa tena mateso, kuumia, kufungwa jela, kunyongwa na hata kufa pia. Waswahili husema kukata tama. Nilishakufa moyo, nikakata tama…. Nikakata mwili, nikabakiza roho ili bibi aje tu aichukue. Lakini moyo wangu ulinituma kufanya jambo… jambo ambalo lingebadilisha historia yangu yote, jambo ambalo kila mwanadamu ambaye angeniona asingenielewa asilani. Kwa nini nife mimi?



Mwaka 1997 ukaanza. Wiki moja kabla ya kufungua shule ndipo nilipoanza kuugua, malaria kali na taifodi zilinibana sana. Niliugua sana mpaka sasa mama akaanza kuhisi dalili za kunipoteza, alianza kuhisi ukweli way ale mambo niliyokuwa namuambia na kuniona kama vile namsimulia hadithi isiyofundisha lolote.



Shule ilipofungua mimi nilishidwa kwenda kwa sababu nilikuwa hoi kitandani, “wakati mwingine ni rahisi mwnadamu kutambua zamu yake inapofika” mimi pia nilitambua zamu yangu sasa. Zilipita siku tatu bila kwenda shule kutokana nah ii hari ya kuumwa. Habari kutoka shuleni zilisema kuwa Ezekiel Chongora na Lusjoy Mgimba pia hawakufika shule, nao pia walikuwa wanaumwa, hiki kitu kilizidi kunishangaza mimi pia.



Siku ya alhamisi ya wiki hiyo hiyo ya kwanza, asubuhi na mapema niliamka nikiwa nina nguvu tele, nilijihisi kuchangamka sana… nilifurahi sana kuona kuna kila dalili ya kupona. Ingawa mwili ulikuwa bado umedhohofu. Ni siku hii ndipo nilopovaa moyo wa ujasili, nikasema lazima nitekeleze lile jambo la kijasiri ambalo nilipanga kulifanya. Nikamwambia mama nataka leo kwenda shule… “Lazima nifike shule leo…! Mama alishituka sana kusikia hivyo kwani na yeye kwa mbaaali sana alishakuwa kaingiwa na hofu juu ya ile hari yangu. Hata hivyo alinizuia kufanya hivyo.



Siku ya ijumaa nikaamka tena nikiwa na ile ile hari ya unafuu, nikafanya maandalizi yangu mapema kabla mama hajaamka na kuondoka zangu kwenda shule, nilijua endapo nitamsubiri atanizuia tena kitu ambacho niliona kama kikwazo kwangu. Nilipofika shule watu walinishangaa sana jinsi nilivyokonda. Fumo sio Fumo tena. Nilikonda na kubakiza mfupa na ngozi. Kwangu nilijiona bado ni jasili sana kujilazimisha kufika hapo mahali ambapo palikuwa kama ni mlango wa kuendea kwa bibi, tena hasa ukizingatia kuwa mwaka huu ulikuwa ni zamu yangu mimi. Na hiki ndio kitu ambacho nilipanga kukifanya, niliona ni lazima niende shule ili watu na marafiki zangu wanione kabla sijafa.



Shuleni nilikutana na Ezekiel Chongola ambaye yeye alikua na afya nzuri tu kwa muonekano, namaanisha hakukonda kabisa, isipokuwa alikuwa na mabaka mengi usoni kwa sababu alikuwa ametoka kuugua ugonjwa wa ‘matetekuwanga’ ugonjwa ambao uliibadili sula yake na kufanya watu wamcheke sana. Lusjoy yeye hakufika bado shule, ilisemekana bado anasumbuliwa kidogo na matezi.



Jioni ilopofika mimi niakrejea nyumbani, nilipofika tu nyumbani ile homa kali ikarejea tena. Sasa ndio ilikuwa kali zaidi…. Mwili ulikuwa unatetemeka sana kama vile roho inataka kuacha mwili…!



Jumapili jioni nikajiona tena nimepata nafuu, hari yangu ikawa haitabiriki kama hari ya hewa, kipindi baridi, kipindi joto, kipindi mvua, kipindi mawingu.



Jumatatu asubuhi kama kawaida niliwahi tena kuamka na kwenda shule, huku nikiwa na nguvu kiasi ila ni mtu aliyekosa furaha. Baadaya ya usafi, mchakamchaka na gwaride la kishule kama kawaida ya jumatatu zote za shule ya Kichangani ikagongwa kengele ya mistalini (Assemble) mida ya saa mbili kamili.



Mwl. Mpako akapita mbele, siku hii ndiyo siku ambayo nilimuona kwa mara ya kwanza akitembea maeneo ya shule bila kubeba fimbo. Baada ya kimya kifupi akatutangazia kuwa “Lusjoy Mgimba amefariki dunia leo hii alfajiri”… “Msiba upo kwao Mafifi na hivyo leo hatutakuwa na masomo…”

 Watu wote tulishtushwa na taarifa hii mbaya na kuanza kulia sana… kila mtu aliyekuwa anamfahamu Lusjoy Mgimba (R.I.P) aligubikwa na majonzi makuu….!! Kwangu mimi ulikuwa ni msiba mkuu zaidi, nililia sana na kujihisi kama ile kura yangu kwake imechangia kutokea kwa hili…!!

Kwa nini nilipiga kura? Nilianza kujiuliza tena aina ya swali lingine, Ezekiel Chongola alinifuata nilipo kaa, akanikumbatia na wote kwa pamoja tukaanza kulia kwa uchungu. Tuliumia sana mioyo. Kamwe sita isahau siku hii katika maisha yangu yote.



Kimwili hauko nasi ila kiroho bado tuko paomja, tutakukumbuka milele daima kaka

Lusjoy Mgimba.



MUNGU AKULAZE MAHALI PEMA PEPONI



*****



This is story, majina yote niliyoyaweka humu ni halisi, anjua haitawavutia watu, hasa hasa wale niliosoma nao primary Kichangani kwa sababu nitakuwa nimewakumbusha Msiba ambao ulituumiza. Lakini nimeandika ili mwenye kujifunza lolote na ajifunze.



The story is true and authentic, japo nime add some salt ili isomeke.



Alpha Amos Ambokile

07147 312028

0767 283131